Ukuaji wa biashara yoyote unategemea na mzunguko wa fedha kwenye
biashara hiyo. Kama mzunguko wa fedha siyo mzuri biashara haiwezi kukua.
Kama mzunguko wa fedha upo vizuri biashara itakua na kutengeneza faida.
Biashara inaposhindwa kutengeneza faida inaelekea kufa. Kuna sababu
nyingi ambazo wafanyabiashara wanaweza kutafuta kwa nini biashara zao
zinakufa. Na mara zote sababu hizi huwa zinakuwa ni za nje. Mambo kama
uchumi haupo vizuri au mabadiliko mengine yamekuwa ndiyo kisingizio cha
biashara kushindwa kufanya vizuri.
Vipi kama leo nikakuambia kwamba kama biashara yako haifanyi vizuri basi
wewe ndiye unayeifanya biashara hiyo ishindwe kwenda vizuri? Utakubali
au utakataa? Kabla hujajipendelea au kujiumiza, angalia sababu hizi tatu
ambazo zinapelekea biashara nyingi kufa na uone kama kuna ambazo
umekuwa unafanya kwenye biashara yako.
Sababu ya kwanza; kutokujua kwa hakika ni kitu gani unachouza.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa na ile dhana kwamba fungua biashara na
watu wakikuona watakuja kununua. Wanaweza kukuona na kuja kununua,
lakini wasirudi tena. Mteja anapokuja kununua kwako mara moja na asije
tena ni dalili mbaya kwa biashara yako.
Mteja anataka kwenda kwenye biashara ambayo yule anayemhudumia anajua
kwa hakika ni kitu gani anachokifanya. Hili linafanywa na
wafanyabiashara wachache mno, wengi wanaendesha biashara zao kwa mazoea.
Wanashindwa kuwashawishi wateja wao kwa nini wanunue kutoka kwao, kwa
sababu hawajui kwa hakika ni namna gani mteja anaweza kunufaika na kile
wanachouza.
Sababu ya pili; kutokujua mteja hasa wa biashara yako ni nani.
Dhana ile ile ya kwamba fungua biashara na watu wataiona, ndiyo imekuwa
inatumika kwamba mteja wa biashara yako ni mtu yeyote. Sikiliza
nikuambie, hakuna biashara ambayo mteja wake ni kila mtu. Kila biashara
ina aina fulani ya wateja wake, ambao ukishawajua hawa kwenye biashara
yako unaweza kuwafikia vizuri na kukuza biashara yako.
Usikazane kumfanya kila mtu awe mteja wako, bali angalia wale ambao
wanaweza kunufaika na kile unachotoa na kisha hakikisha hao ndiyo
unawafikia vizuri na kufanya nao biashara.
Sababu ya tatu; kuchelewa kubadilika.
Biashara ambazo zilikuwa zinavuma sana miaka kumi iliyopita sasa hivi
nyingi hazipo. Biashara tunazoona leo ndiyo bora sana, miaka kumi ijayo
zinaweza zisiwepo kabisa. Unachopaswa kuelewa ni kwamba mabadiliko
yanatokea, na yanatokea kwa kasi kubwa sana. Wafanyabiashara
wanaoshindwa kwenda na kasi hii ya mabadiliko yanawaacha nyuma na
kushindwa kukuza biashara zao.
Unapokuwa mfanyabiashara, unahitaji kuwa karibu sana na biashara yako,
hapa ndipo unapoweza kuyaona mabadiliko yanayoathiri biashara yako moja
kwa moja.
Wewe kama mpenda biashara, hakikisha mambo haya matatu hayawi kikwazo kwenye ukuaji wa biashara yako.
Thursday, August 11, 2016
Home »
UJASILIAMALI
» Makosa Matatu Yanayowakosesha Wafanyabiashara Wengi Faida
0 comments:
Post a Comment