Thursday, August 25, 2016

FAHAMU KILIMO BORA CHA MPUNGA CHA UMWAGILIAJI


Maandalizi sahihi ya shamba ni jambo la msingi katika kuboresha kilimo cha umwagiliaji wa mpunga. shamba lisipoandaliwa vema husababisha mbinu bora zinazoshauriwa kutoonyesha matokeo katika kiwango kinachotarajiwa hasa katika uzalishaji. Kimsingi maandalizi ya shamba yanatakiwa yafanyike kwa usahihi
na kwa wakati katika mtiririko unaotakiwa. Zifuatazo ni hatua saba muhimu na za msingi katika kilimo cha mpunga

1. KUSAFISHA SHAMBA
Safisha shamba mapema kabla ya msimu kuanza. Kusanya na kuangamiza visiki na takataka nyingine zote. Masalia ya mazao yanaweza kutumika kutengeneza mbolea  ya mboji. Inapobidi tumia moto kwa uangalifu sana maana moto unaweza kuharibu mazingira, unaua wadudu rafiki, unaharibu udongo na kuteketeza mboji.

2. KULIMA
Kulima husaidia kupunguza kiasi cha magugu, huruhusu mzunguko mzuri wa hewa na maji, hurahisisha mizizi kupenya na kuchanganya masalia ya mazao kwenye ardhi. Wakati wa kulima uangalifu unahitajika ili kuzuia kuharibu usawa wa ardhi. Kina cha kulima kiwe kati ya sentimeta 10 na 15. Ili kurahisisha na kuharakisha kazi ya kulima ni vema kutumia zana/mashine rahisi kama Trekta la mkono na wanyamakazi 

3. KUKARABATI/KUJENGA MAJARUBA
Baada ya kulima hakikisha kuwa kingo za jaruba zimekarabatiwa ili kuweza kuhifadhi maji vema. Kama ni shamba jipya, ujenzi wa kingo za jaruba  ufanyike kwa kufuata utaalamu unaotolewa. Kingo imara ni muhimu kudhibiti vema maji shambani. 
 
4. KUVURUGA
Weka maji shambani kiasi cha sentimeta 3 hadi 5 juu ya usawa wa ardhi ili kukamilisha vema uvurugaji. Jembe la mkono linatumika lakini ili kurahisisha na kuharakisha kazi hii ni vema kutumia trekta la mkono au wanyamakazi. Unapotumia wanyamakazi au trekta la mkono weka maji shambani si zaidi ya siku moja kabla. Shamba lililovurugwa vema huiwezesha mizizi ya miche kupenya vema ardhini.

5. KUSAWAZISHA SHAMBA
Baada ya kuvuruga ni lazima kuhakikisha kwamba shamba limesawazishwa vema. Shamba lililosawazishwa vema linaruhusu usambaaji mzuri  wa maji. Wakati wa kusawazisha kina cha maji kiwe kiasi cha sentimeta 3-5 juu ya usawa wa ardhi Ili kurahisha kazi hii tumia reki ya ubao ili kuvuta udongo kutoka sehemu zilizoinuka kuelekea sehemu zilizo bondeni

6.VYANZO NA ATHARI ZA UPOTEVU WA MAJI YA UMWAGILIAJI
Ili kupata maji ya kutosha inabidi kuhakikisha kwamba upotevu wa maji ya umwagiliaji unapungua kwa kiwango kikubwa na wakulima wanamwagilia maji kwa kiasi kinachohitajika bila kuzidisha kiwango.

Vyanzo vya upotevu wa maji ya umwagiliaji katika skimu za mfano ni pamoja na:
•  Maji yanayopotea kwenye mifereji mikuu, ya kati na ile midogo ya kusambaza maji mashambani.
•  Maji yanayopotea mashambani wakati wa kumwagilia.

Upotevu wa maji kwenye mifereji mikuu, ya kati na ile ya kusambaza maji unasababishwa na aina ya udongo uliotengeneza kingo za mfereji, uchafu na matengenezo hafifu ya mifereji.  Katika baadhi ya skimu upotevu wa maji kwenye mfereji mkuu uliosababishwa na kuvuja maji kwenye tuta la mfereji mkuu na kunywea chini ya ardhi ulikuwa mkubwa kiasi cha kuathiri upatikanaji wa maji kwenye  mashamba yaliyoko mbali na banio.Vilevile athari nyingine ilikuwa ni maji mengi kuingia sehemu yasikohitajika na kusababisha tatizo la maji kutuama kwa muda mrefu.Hivyo wakulima wanashauriwa kupunguza upotevu huu wa maji kwenye mfereji kwa kujengea na kusakafia. Upotevu wa maji mashambani wakati wa kumwagilia unasababishwa na kuvuja kwenye tuta linalozunguka jaruba, kunywea chini na kuzidisha kiwango cha maji ya kumwagilia kinachotakiwa. Hii mara nyingi inasababishwa na utengenezaji mbovu wa jaruba. utengenezaji wa majaruba na uimarishaji wa kingo za jaruba umesaidia kupunguza upotevu wa maji kwa kiwango kikubwa na hatimaye kuongeza mavuno na kipato cha mkulima. 

7. UPANDIKIZAJI MPUNGA
Ili kupata mavuno mengi na kukifanya kilimo cha mpunga kuwa cha faida ni muhimu  wakulima kuzingatia mbinu hii muhimu na kuachana na kilimo cha kiholela kwa kumwaga mbegu moja kwa moja shambani. Aidha kwa wakulima wanaofuata kanuni hii wamepata mafanikio makubwa. 

Faida zinazopatikana kwa kupandikiza mpunga
•  Mkulima huweza kuchagua miche bora na mizuri ikiwa  kitaluni.

•  Miche hukua haraka na yenye afya .
•  Kiasi kidogo cha mbegu huhitajika.
•  Mavuno huwa mengi.
Njia  za kupandikiza miche ya mpunga
Zipo njia kuu mbili za kupandikiza miche ya mpunga, nazo ni: 
•  Kupandikiza kwa mistari
•  Kupandikiza bila ya kufuata mistari (Mchaka mchaka).
Aidha kati ya njia hizi mbili, njia ya kupanda kwa mistari ndiyo inayopendekezwa.zaidi. Pamoja na kwamba upandikizaji wa mistari unahitaji nguvu kazi zaidi, njia hii imeonyesha kuwa na mafaniko mengi ikilinganishwa na kupandikiza kiholela. Shamba lililopandwa kwa mistari ni rahisi kupalilia kwa kutumia kipalizi cha  kusukuma kwa mkono. Pia ni rahisi kwa mkulima  kupanga idadi ya mashina/mimea kwa eneo kwa  uchagua nafasi aitakayo itakayompa mazao mengi.

Uandaaji wa miche
Kabla ya kupandikiza miche shambani ni muhimu kufanya maandalizi yafuatayo:  
•  Inashauriwa kumwagilia miche kwanza ili kupata urahisi wa kungo’a
•  Ili kuzuia miche isikatike ovyo, miche ing’olewe kwa kushikwa chini zaidi ya shina
•  Epuka kung’oa miche mingi kwa wakati mmoja
•  Miche ifungwe kwenye mafungu madogo madogo ili kurahisisha usafirishaji na upandikizaji  shambani
•  Miche bora tu ndio ichaguliwe. Sifa za miche bora
•  Iwe na kimo kinacholingana, 
•  Iwe na majani mafupi yaliyosimama, yenye mizizi mingi na yenye afya, isiyoshambuliwa na wadudu wala magonjwa, 
Jinsi ya kupandikiza miche
•  Miche ishikwe  kwa vidole vitatu kama inavyoosha kweye picha chini 
•  Pandikiza kati ya miche 2 -3 kwa kila shina
•  Kwa mafanikio zaidi, miche ipandikizwe katika kina cha sentimita 2-3.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Blog Archive

Latest Posts

Translate

Popular Posts

Blog Archive

Recent Posts

Unordered List

Pages

Theme Support