Kitunguu hutumika kama kiungo cha kuongeza ladha kwenye chakula, na pia hutumika kama dawa ya kansa ya tumbo, vidonda na majipu.
Ustawi
Zao la vitunguu hustawi katika udongo wa tifu tifu wenye mbolea ya kutosha, ukiwa na uchachu wa udongo (PH) kiasi cha 6 – 6.8. Udongo wa mfinyanzi haufai kwa zao la vitunguu kwa kuwa hauruhusu viazi vya vitunguu (bulbs) kutanuka. Hivyo uwezekano wa kupata mazao ni mdogo. Pia udongo wa kichanga haufai kwa zao la kitunguu kwa kuwa hauna mbolea na hivyo vitunguu huwa vidogo sana, jambo ambalo ni vigumu kupata mazao yanayofaa kwa soko.
Zao la kitunguu huhitaji unyevu muda wote wa ukuaji wake. Zao hili lina mizizi mifupi hivyo linahitaji kumwagiliwa maji mara kwa mara.
Aina za vitunguu
Kuna aina mbili za vitunguu ambazo zimezoeleka:
• Vitunguu vya asili kama vile Singida, na Rujewa (aina hii ina rangi ya kahawia iliyopauka).
• Chotara: Hii ni aina ya vitunguu inayojulikana kama vitunguu vya kisasa. Katika kundi hili kuna vitunguu kama Texas grano, Red creole, Bombay red, White granex, na Super rex.
Mgawanyiko
Zao la vitunguu limegawanyika katika makundi mawili. Hii inatokana na uhitaji wa mwanga na ukuaji wake. Aina ya kwanza inahitaji mwanga kwa saa 8-13 ili kuweza kuchanua na kutoa mbegu.
Aina ya pili inahitaji mwanga kwa saa 13-15 kuweza kuchanua na kutoa mbegu.
Kupanda
Vitunguu hupandwa kwa kutumia mbegu ambazo husiwa kwenye vitalu. Kitalu kinaweza kuwa na upana wa mita 1, urefu unategemeana na ukubwa wa eneo ulilo nalo.
Unaweza kupanda vitunguu kwenye matuta mbonyeo (Sunken bed). Aina hii ya upandaji hutumika kwenye eneo lenye shida ya maji. Upana wa tuta uwe mita moja.
Kupanda kwenye matuta mwinuko (Raised bed) upandaji wa iana hii hutu mika sehemu yenye maji mengi au yanayotuama.
Tahadhari: Maji yakituama kwenye vitunguu hufanya vitunguu kuoza, hivyo kuathiri mavuno.
Nafasi
Vitunguu vipandwe kwa nafasi ya sentimita 7.5 kutoka mche hadi mche, sentimita 12.5 kutoka mstari mmoja hadi mwingine kwenye matuta.
Mbole ya kupandia
Unaweza kutumia mboji, au samadi iliyo oza vizuri kupandia. Baada ya hapo unaweza kuongeza mboji baada ya miezi miwili. Endapo unafanya kilimo kisichozingatia misingi ya kilimo hai, unaweza kupanda kwa kutumia mbolea aina ya NPK (20:10:10) baada ya mwezi na nusu, unaweka mbolea ya Urea.
Palizi
Vitunguu ni zao lenye uwezo mdogo sana wa kushinda na magugu. Hivyo, inabidi shamba liwe safi muda wote wa ukuaji hadi kuvuna.
Uvunaji
Kwa kawaida, vitunguu huchukua muda wa miezi 5-6 tangu kupandwa hadi kuvunwa. Unaweza kuanza kuvuna vitunguu baada ya asilimia 75 ya shingo za vitunguu kuvunjika. Baada ya kuvuna, unaweza kuweka kwenye madaraja (grades) kwa kufuata ukubwa, rangi na unene wa shingo ya kitunguu. Vitunguu vyenye shingo nyembamba hudumu zaidi, vyenye shingo nene huoza haraka.
Ukataji
Hakikisha kuwa shingo ya kitunguu inabaki kiasi cha sentimita 2. Hii husaidia kuzuia kuoza haraka.
Namna ya kuhifadhi vitunguu
Baada ya kuvuna, hifadhi vitunguu kwenye kichanja chini ya kivuli na uvitandaze vizuri. Unaweza kuhifadhi vitunguu kwa kufunga kwenye mafungu na kuvitundika. Vitunguu vikihifadhiwa vizuri vinaweza kukaa hadi miezi minne bila kuharibika, hii hutegemeana na aina ya uhifadhi.
Wadudu wanaoshambulia vitunguu
Kuna aina nyingi za wadudu wanaoweza kushambulia vitunguu. Hawa wafuatao ni baadhi ya wadudu waliozoeleka kwenye zao la vitunguu.
Thiripi (Thrips): Wadudu hawa hukaa kwenye jani sehemu inayokutana na shina. Wadudu hawa hufyonza maji kwenye majani ya vitunguu na kusababisha majani kuwa na doti nyeupe.
Madhara: Husababisha vitunguu kudumaa hivyo kuathiri ukuaji wake jambo ambalo huathiri mavuno pia.
Minyoo fundo (Nematodes): Aina hii ya minyoo hushambulia mizizi ya vitunguu. Hali hii husababisha kudumaa kwa vitunguu kwa kuwa hushindwa kufyonza maji na chakula kutoka ardhini.
Vidomozi (Leaf minor): Hushambulia majani kwa kujipenyeza kwenye ngozi ya jani na kusababisha michoro ambayo huathiri utendaji wa majani.
Utitiri mwekundu (Red spider mites): Wadudu hawa hufyonza maji kwenye majani na kusababisha vitunguu kunyauka.
Funza wakatao miche: Funza hawa hutokana na wadudu wajulikanao kama Nondo, na hushambulia shina na kulikata kabisa.
Namna ya kukabiliana na wadudu hawa
Unaweza kukabiliana na wadudu hawa kwa kufanya kilimo cha mzunguko. Usioteshe vitunguu sehemu moja kwa muda mrefu, au kufuatanisha mazao jamii ya vitunguu kama vile leaks.
Tumia mbegu bora zilizothibitishwa kutoka kwenye kampuni zinatambuliwa kisheria na kibiashara. Kupanda kwa wakati unaotakiwa; vitunguu visipandwe wakati wa kiangazi. Vipandwe wakati wa majira ya baridi na kuvunwa wakati wa joto. Tumia dawa za asili za kuulia wadudu, au dawa nyinginezo zinazopendekezwa na wataalamu wa kilimo.
1. Purple blotch: Ugonjwa huu husababishwa na ukungu (fungus). Ugonjwa huu husababisha mabaka ya zambarau na meusi katika majani ya vitunguu. Ugonjwa huu hutokea wakati wa unyevu unyevu mwingi.
Madhara: Ugonjwa huu hupunguza mavuno mpaka asilimia hamsini (50%).
2. Stemphylium leaf blight: Hukausha majani kuanzia kwenye ncha hadio kwenye shina.; Ugonjwa huu hutokea wakati wa unyevu na ukungu mwingi.
Madhara: Hupunguza mavuno hadi kwa asilimia sabini na tano (75%).
3. Magonjwa ya virusi (Onion yellow draft virus): Ugonjwa huu husababisha vitunguu kuwa na rangi iliyochanganyika, kijani na michirizi myeupe au njano. Vitunguu hudumaa kwa kiasi kikubwa;Ugonjwa huu husababishwa na kimamba.
Madhara: Huathiri mavuno kwa asilimia 80 mpaka asilimia 100%.
4. Kuoza kwa kiazi (Bulb rot): Husababishwa na fangasi. Ugonjwa huu hutokea vitunguu vikishakomaa, huku udongo ukiwa na maji maji. Vitunguu vikishakomaa visimwagiliwe tena.
Uharibifu wa vitunguu usiotokana na magonjwa
1. Kuchipua baada ya kuvunwa: Hali hii hutokea endapo vitunguu vitavunwa kabla ya muda wake. Endapo vitunguu havitakaushwa vizuri baada ya kuvunwa. Hali hii husababisha uharibifu mpaka asilimia themanini (80%). Sehemu ya kukaushia vitunguu iwe na hewa inayozunguka na mwanga wa kutosha. Vitunguu vikiwekwa gizani huchipua kwa urahisi.
2. Muozo laini (Soft rot): Ugonjwa huu hushambulia vitunguu baada ya kukomaa; husababishwa na vimelea (bacteria). Vitunguu hutoa harufu mbaya ya uozo. Kuepuka hilo vuna kwa wakati unaofaa, hifadhi sehemu yenye mwanga na hewa inayozunguka.
Virusi
Unaweza kuzuia vimamba ambao ndio wanaoeneza virusi kwa kutumia dawa za kuulia wadudu.
Vitunguu vinalipa
“Vitunguu vinatofauti kidogo na mazao mengine ya mboga mboga kwa kuwa si
rahisi kukosa soko, na endapo bei si nzuri unaweza kuhifadhi kwa muda
ili kusubiri bei iwe nzuri.” Ni maneno ya mkulima Peniel Rodrick
(pichani) ambaye amejikita zaidi katika kilimo cha vitunguu kibiashara.
Mkulima huyu kutoka kijiji cha Oloigeruno anasema pamoja na kwamba
anazalisha pia mazao mengine, lakini ameamua kujikita zaidi kwenye
vitunguu baada ya kugundua siri na namna ya kupata faida zaidi.
Toka aanze kilimo cha vitunguu miaka 12 iliyopita, ameweza kuendesha
maisha yake vizuri, ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi mingine kama
ufugaji wa ng’ombe, kujenga nyumba ya kisasa na kuitunza familia yake ya
watoto watatu ipasavyo. Pamoja na hayo anasema tatizo kubwa la vitunguu
ni magonjwa na wadudu. Anasema si rahisi sana kugundua mara moja kuwa
kuna ugonjwa unaoshambulia vitunguu, na mara unapogundua unakuwa
umefikia kwenye hali mbaya.
0 comments:
Post a Comment