Friday, August 12, 2016

FAHAMU KILIMO BORA CHA ALIZETI

Image result for alizeti

Utangulizi

Alizeti ni zao mojawapo kati ya mazao muhimu yanayotoa mbegu za mafuta. Hutoa mafuta kati ya asilimia 40 – 45 na mashudu yake ni chakula cha mifugo. Alizeti huvumilia ukame na hulimwa kwa ajili ya biashara na matumizi ya nyumbani. Wakulima huvuna kiasi kidogo, kati ya gunia 3 – 5 kwa hekta. Hivyo kwa mavuno mengi na bora, mkulima anashauriwa kuzingatia mambo yafuatayo:-

Kuandaa Shamba

Unashauriwa kutayarisha shamba lako mapema kwa kukatua ardhi na kulainisha vizuri. Samadi yaweza kuchanganywa vizuri na udongo wakati wa kuandaa shamba.
www.ariuyole.go.tz

Wakati wa Kupanda

Upandaji wa alizeti hutegemea sana hali ya hewa ya eneo husika.
Maeneo yenye mvua nyingi alizeti huanza kupandwa mwishoni mwa mwezi Januari mpaka katikati ya
mwezi Februari.
Maeneo yenye mvua kidogo alizeti hupandwa mwezi Desemba hadi Januari.

Kiasi cha mbegu na upandaji

Kiasi cha kilo 3 – 4 za mbegu zinatosha kupanda eneo la ekari moja.
Panda mbegu 3 – 4 katika kila shimo moja kwa nafasi ya sentimita 75 kutoka mstari hadi mstari na sentimita 30 kutoka shimo hadi shimo. Shimo la mbegu liwe na kina cha sentimita 2.5 – 5.
Wiki mbili baada ya kuota, punguza miche katika kila shimo na kubakiza mche mmoja.

Kiasi cha mbolea

Mbolea zinazofaa kwa kilimo cha alizeti ni zile za kupandia na kukuzia hasa kwenye maeneo yasiyo na rutuba.
Wakati wa kupanda tumia nusu mfuko kwa ekari moja ya mbolea ya kupandia na mfuko mmoja kwa ekari moja ya mbolea ya kukuzia kwa kuigawa mbolea hiyo mara mbili. Nusu ya kwanza iwekwe wakati wa kupanda na nusu ya pili iwekwe wiki mbili baadaye.
Wakati wa kuweka mbolea angalia isigusane na mbegu au mche wa alizeti kwani huunguza.

Palizi

Alizeti hukua taratibu katika wiki chache za mwanzo. Hivyo unashauriwa kupalilia mapema ili kupunguza
hasara. Katika maeneo yaliyo na magugu machache, palizi moja tu inatosha. Vile vile maeneo yenye upepo
mkali, wakati wa kupalilia inulia matuta ili kuzuia kuanguka.

Wanyama na wadudu Ndege

Alizeti hushambuliwa sana na ndege ambao huweza kuteketeza hadi asilimia 50 ya mazao shambani.

Kuzuia

- Usipande alizeti karibu na msitu/pori
- Vuna mapema mazao yako mara tu kichwa kinapobadilika rangi na kuwa manjano
- Panda alizeti kwa wingi katika shamba moja
- Amia ndege kwa mutumia sanamu, makopo na ua kuweka watu ingawa ni gharama.

Funza wa vitumba (American bollworm)

Funza huyu hutoboa mbegu changa kuanzia mara tu vitumba vya maua vikifunguka mpaka karibu na
kukomaa kwa mbegu.

Kuzuia:

- Tumia dawa yo yote ya kuulia wadudu inayopatikana katika eneo lako.
Magonjwa
Alizeti hushambuliwa na magonjwa yakiwemo madoa ya majani, kutu, kuoza kwa mizizi, shina, 
 

kichwa na kushambuliwa na virusi.


www.ariuyole.go.tz

Kuzuia:

- Tumia kilimo cha mzunguko wa mazao
- Panda mbegu safi zilizothibitishwa na wataalamu
- Choma masalia ya msimu uliopita

Uvunaji

Unashauriwa kuvuna alizeti mara tu inapokomaa ili kupunguza hasara ya kushambuliwa na ndege. Alizeti iliyokomaa kichwa hubadilika rangi toka kijani kibichi na kuwa njano. Kata vichwa na kuvianika juani ili vikauke vizuri.
Piga piga vichwa ili kutoa mbegu za alizeti, kisha upepete na kuendelea kuzianika ili zikauke vizuri.
Utafiti unaonyesha kuwa mkulima anaweza kupata magunia kati ya 10 -12 kutoka katika ekari moja.

Kwa Mawasiliano zaidi wasiliana na:

Taasisi ya Utafiti Uyole,
Kitengo cha mbegu za Mafuta
S.L.P. 400
MBEYA
Simu: 025 2510062
Fax: 025 2510065
Barua pepe; ariuyole@iwayafrica.com
website: www.ariuyole.go.tz
www.ariuyole.go.tz
Share:

0 comments:

Post a Comment

Blog Archive

Latest Posts

Translate

Popular Posts

Blog Archive

Recent Posts

Unordered List

Pages

Theme Support